SectionsExitTanzania

Tanzania

Ordinary Time,Ordinary Time,Ordinary Time,MarianExit
Verse 1

Mwenyezi Mungu Rahimu na mradhi mwema,

salamu salamu Mwumba wa Adamu

Watanzania tumekuja kwa wimbo,

na tenzi kuongea nawe leo hii

Uchaguzi mkuu huu tunaoandaa,

twaomba ujae baraka zako kuu

Kusudi uwepo wako udhihirike,

katika serikali tutakayounda

Verse 2

Rais mpya awe fimbo bora,

awe taa ya kweli kwenye kinara

Wabunge wawe matawi mazuri,

yenye kuzaa kwenye mti wa rutuba

Madiwani wawe watu wa watu,

kuongoza watu kwa ajili ya watu

Tujenge Tanzania madhubuti,

mioyoni badala ya ardhini

Verse 3

Wagonjwa wapone, makiwa wafarijiwe,

masikini waonje maziwa kila siku

Wajane waishi, yatima waende shule,

fukara waone thamani ya utu wao

Majanga yakome, majeruhi watibiwe,

walio gerezani wawe huru mitaani

Undugu ukue, amani iongezeke,

na wahalifu wote wabadilishe tabia

Verse 4

Na watoto, watoto wadogo,

walelewe kwa maadili

Madhehebu, yote ya kidini,

yawe tahadhari ya upendo

Navyo vyama, vyetu vya siasa,

viwe siri kuu ya amani

Ibilisi, afunge virago,

aondoke kamwe asirudi!n

Verse 5

Kiapo atakachoapa rais mpya,

kidumu hata hatimamu ya dahari

Majaribu yote yatakayotukumbuka,

yapimwe yasizidi kimo chetu

Mwenyezi Mungu rahimu twakuomba,

tulinde tulinde bila ya kuchoka

Ili mwisho wa safari ya hapa,

tufike mbinguni wote Tanzania

Comments

Sign in to join the conversation

Share your thoughts on this hymn with the community.